Baada ya kuthibitishwa kwa uwanja wa mechi, Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limetangaza uteuzi rasmi wa waamuzi kwa fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF.
CAF imemteua mwamuzi wa kimataifa kutoka Mauritania, Dahane Beida, kuwa mwamuzi wa kati katika mchezo wa marudiano wa fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF kati ya Simba SC ya Tanzania na RS Berkane ya Morocco. Mchezo huo umepangwa kufanyika tarehe 25 Mei 2025 katika Uwanja wa Amaan Zanzibar.
Dahane Beida ni mwamuzi mwenye uzoefu mkubwa katika soka la Afrika. Miongoni mwa mechi kubwa alizowahi kuzisimamia ni fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2023 kati ya Ivory Coast na Nigeria. Pia, alisimamia mechi ya marudiano ya fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF msimu wa 2022/23.
Fainali ya mwaka huu inatarajiwa kuwa ya kusisimua, kwani Simba SC itakuwa inacheza fainali yake ya kwanza ya Kombe la Shirikisho, huku RS Berkane wakitafuta taji lao la tatu katika mashindano haya, baada ya kulibeba mwaka 2020 na 2022.
Mchezo wa kwanza wa fainali hiyo utafanyika tarehe 17 Mei 2025 katika Uwanja wa Berkane Municipal, Morocco.
