Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Monday, March 30, 2026

AFISA ZIMAMOTO MBEYA AWAPA TABASAMU WAHITAJI

 










Na Joachim Nyambo,Mbeya

Afisa Habari Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mbeya Sajenti Esther Dismas Kinyaga ambaye pia ni Makamu Mkuu wa Idara ya Uhitaji Maafa na Makundi Maalum Taifa (SMAUJATA), ameacha alama ya matumaini na faraja baada ya kushiriki kama mgeni rasmi katika ziara ya kutembelea kituo cha kulea watu wenye ulemavu kilichopo Iyunga, Jijini Mbeya.

Ziara hiyo imeandaliwa na kundi la Mbeya Generation, ikiwa na lengo la kuwafariji na kuwatia moyo watoto wenye ulemavu wanaolelewa katika kituo hicho, pamoja na kuihamasisha jamii juu ya umuhimu wa kuwajali na kuwaunga mkono.
Akizungumza katika tukio hilo, Sajenti Kinyaga alitoa mafunzo ya kuwaimarisha kisaikolojia kwa watoto hao na walezi wao, akisisitiza umuhimu wa kujithamini, kuwa na matumaini na kujiamini licha ya changamoto zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku.
“Ulemavu sio mwisho wa maisha, kila mmoja ana thamani yake katika jamii hivyo ni muhimu kuendelea kupambana na kutumia fursa zilizopo kujijenga na kutimiza ndoto zenu,” alisisitiza Kinyaga.
Aidha aliwataka wananchi na wadau mbalimbali kuendelea kuwaunga mkono watu wenye ulemavu kwa vitendo, ikiwemo kuwapatia mahitaji muhimu na kuhakikisha wanapata fursa sawa katika nyanja zote za maisha.
Katika kuonesha upendo na mshikamano, Sajenti Kinyaga alikabidhi zawadi mbalimbali kwa watoto hao hatua iliyowaletea furaha na tabasamu huku ikionyesha umuhimu wa kugusana na jamii zinazohitaji msaada.
Tukio hilo limeacha kumbukumbu ya kipekee ya upendo, mshikamano na matumaini mapya kwa watoto hao pamoja na walezi wao, likiwa ni chachu ya kuendelea kuhamasisha jamii kujenga moyo wa kujali na kusaidiana.

MWENYEKITI JUMUIYA YA WAZAZI CCM MBEYA MJINI ATOA JEZI KWA WASHINDI LIGI YA WANAWAKE

 





Na Joachim Nyambo,Mbeya

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbeya Mjini, Emmanuel Mwalupindi amekabidhi zawadi ya jezi kwa timu ya Icons Queens iliyofanya vizuri na kuibuka washindi katika ligi ya wanawake mkoani Mbeya, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha na kuendeleza michezo kwa wanawake.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo, Mwalupindi amesema kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya kuwawezesha wanawake kijamii na kiuchumi, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika sekta hiyo ili kukuza vipaji vya vijana wa kike.

Ameongeza kuwa Jumuiya ya Wazazi itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wanawake wanapata fursa zaidi za kushiriki katika michezo na kuonesha uwezo wao, jambo litakalosaidia kuinua hadhi ya michezo ya wanawake katika ngazi ya mkoa na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wao, baadhi ya wachezaji wa timu hiyo wameeleza kufurahishwa na zawadi hiyo, wakisema kuwa imewapa motisha ya kuendelea kufanya vizuri zaidi katika mashindano yajayo. Wameomba wadau wengine kujitokeza kusaidia maendeleo ya michezo ya wanawake ili kufikia mafanikio makubwa zaidi.

Ligi hiyo ya wanawake mkoani Mbeya imekuwa chachu ya kugundua na kukuza vipaji vya soka kwa wanawake, huku ikitoa fursa kwa timu mbalimbali kushiriki na kujenga ushindani wenye tija.

Friday, March 13, 2026

KAMATI YA BUNGE YA MAJI NA MAZINGIRA YATUA IRINGA






Sehemu ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Maji na Mazingira baada ya kuwasili mkoani Iringa

Na Mwandishi Wetu

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Jackson Kiswaga Machi 12, 2026 imewasili katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa ajili ya ziara ya kutembelea Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR) unatekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) katika Halmashauri ya Iringa.

Wajumbe hao wameambatana na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Festo Dugange, Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Balozi Baraka Luvanda na watendaji kutoka Ofisi hiyo.

Akizungumza, Dkt. Dugange alisema mradi huo unawezesha wananchi kufanya shughuli za kiuchumi bila kuathiri mazingira.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James alipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa utekelezaji wa mradi huo na kusema unasaidia kulinda mazingira.

Mradi huo pia unatekelezwa katika Halmashauri za Wilaya za Wanging’ombe, Mbarali na Mbeya katika bonde la Ruaha Mkuu na halmashauri za Sumbawanga, Mpimbwe na Tanganyika katika Bonde la Ziwa Rukwa.