Na Joachim Nyambo,Mbeya
Afisa Habari Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mbeya Sajenti Esther Dismas Kinyaga ambaye pia ni Makamu Mkuu wa Idara ya Uhitaji Maafa na Makundi Maalum Taifa (SMAUJATA), ameacha alama ya matumaini na faraja baada ya kushiriki kama mgeni rasmi katika ziara ya kutembelea kituo cha kulea watu wenye ulemavu kilichopo Iyunga, Jijini Mbeya.
Ziara hiyo imeandaliwa na kundi la Mbeya Generation, ikiwa na lengo la kuwafariji na kuwatia moyo watoto wenye ulemavu wanaolelewa katika kituo hicho, pamoja na kuihamasisha jamii juu ya umuhimu wa kuwajali na kuwaunga mkono.
Akizungumza katika tukio hilo, Sajenti Kinyaga alitoa mafunzo ya kuwaimarisha kisaikolojia kwa watoto hao na walezi wao, akisisitiza umuhimu wa kujithamini, kuwa na matumaini na kujiamini licha ya changamoto zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku.
“Ulemavu sio mwisho wa maisha, kila mmoja ana thamani yake katika jamii hivyo ni muhimu kuendelea kupambana na kutumia fursa zilizopo kujijenga na kutimiza ndoto zenu,” alisisitiza Kinyaga.
Aidha aliwataka wananchi na wadau mbalimbali kuendelea kuwaunga mkono watu wenye ulemavu kwa vitendo, ikiwemo kuwapatia mahitaji muhimu na kuhakikisha wanapata fursa sawa katika nyanja zote za maisha.
Katika kuonesha upendo na mshikamano, Sajenti Kinyaga alikabidhi zawadi mbalimbali kwa watoto hao hatua iliyowaletea furaha na tabasamu huku ikionyesha umuhimu wa kugusana na jamii zinazohitaji msaada.
Tukio hilo limeacha kumbukumbu ya kipekee ya upendo, mshikamano na matumaini mapya kwa watoto hao pamoja na walezi wao, likiwa ni chachu ya kuendelea kuhamasisha jamii kujenga moyo wa kujali na kusaidiana.









No comments:
Post a Comment