Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Sunday, April 12, 2026

MBARALI WAJIPANGA USHINDANI SHIMISEMITA 2026

 









Na Mwandishi Wetu

 

HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya imesema imejizatiti kuja na timu bora kwenye Mashindano  ya Shirikisho la Michezo ya Serikali za Mitaa nchini(Shimisemita) yanayotarajiwa kufanyika mkoani Mbeya Septemba mwaka huu.

 

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Idara ya Michezo, Sanaa na Utamaduni, Mariam Mnozya alipokuwa akifunga bonanza la Michezo lililowakutanisha watumishi wa halmashauri hiyo huku pia timu za Tanesco na Magereza zikishiriki kama waalikwa.

 

Watumishi walioshiriki bonanza hilo la michezo lililofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Rujewa ni kutoka Kata tano za Tarafa ya Rujewa ambazo ni Rujewa , Lugelele ,Imalilo songwe , Ubaruku na Mawindi.

 

Katika bonanza hilo, Mnozya amesisitiza umuhimu wa watumishi  kuzingatia mazoezi ya mara kwa mara ili kufanya miili yao kuwa sawa na tayari kwa mashindano ya Shimisemita.

 

Amesema pamoja na kuimarisha miili kiafya ni muhimu watumishi wa halmashauri hiyo kama ilivyo kwa wenzao wa halmashauri zote za Mkoa wa Mbeya kuzingatia mazoezi ili kuleta ushindani kwenye mashindano ya Shimisemita mwaka huu kwakuwa ndiyo watakuwa wenyeji.

 

"Kama tunavyojua sisi ni wachezaji lazima tufanye mazoezi ili kuhakikisha tunakuwa  na timu bora zitakazoweza kushindana na kutoa changamoto kwa wapinzani.Mazoezi haya yasiishie hapa tuendelee kufanya mara kwa mara maana mashindano ya mwaka huu sisi kama Mkoa wa Mbeya ni wenyeji wa hivyo hatuwezi kukubali kutoka kwa aibu. "  amesisitiza Mnozya

 

Bonanza hilo lenye lengo la kuibua vipaji vya wachezaji watakaounda Timu ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali itakayokwenda kushiriki michuano ya Shimisemita mwaka huu lilihusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, kikapu ,mikono, wavu, pete, bao na karata.

No comments:

Post a Comment