Na Mwandishi Wetu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga amewataka wanavyuo mkoani Mbeya kujiepusha na vitendo visivyofaa katika jamii ikiwemo uhalifu.
Hayo ameyasema Novemba 14, 2024 wakati akifungua mashindano ya mpira wa miguu yanayohusisha vyuo vikuu mkoani humo yanayojulikana kama "Dreams Intercollege" yaliyofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Mwenge Jijini Mbeya.
Aliongeza kuwa, mashindano hayo yakawe chachu katika kuibua vipaji vya mpira wa miguu kwa wanavyuo mkoani humo kwani michezo ni ajira hivyo alisisitiza kutumia vizuri fursa ya kuanzishwa kwa mashindano hayo.
Naye, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Mbeya Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Veronica Ponera amewataka wanavyuo mkoani humo kujiepusha na ukatili wa kijinsia, kujiepusha na tamaa ya vitu vya thamani ambavyo vinaweza kuwaingiza kwenye vishawishi vya vitendo viovu.
"Jeshi la Polisi nchini linaendelea na kampeni ya Tuwaambie kabla hawajaharibiwa hivyo ni nafasi kwetu kuwaeleza wanavyuo mambo ya kujiepusha nayo kabla hamjaharibikiwa na kupoteza dira ya kufikia ndoto zenu" alisema ASP Ponera.
Awali akizungumza Mratibu wa mashindano hayo Meneja wa kituo cha redio"Dreams fm" cha Jijini Mbeya ndugu Samuel Mhina amesema kuwa mashindano hayo yatashirikisha wanavyuo wote waliopo mkoani Mbeya, T.I.A ambaye ni bingwa mtetezi, CUoM, Tumaini, MUST, Chuo cha Afya - Ifisi yakiwa na lengo la kujenga umoja na kuibua vipaji.
Mechi ya ufunguzi ambayo iliwakutanisha chuo kikuu cha katoliki Mbeya (CUoM) dhidi ya T.I.A imemalizika kwa kushuhudia CUoM ikiibuka na ushindi wa magoli matano kwa bila na kukabidhiwa ngao ya jamii ikiwa ni ishara ya ufunguzi wa mashindano hayo.



No comments:
Post a Comment