Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Monday, October 5, 2026

Umuhimu wa Viongozi wa Dini watajwa kwenye PJT-MMMAM

 








Na Mwandishi Wetu,Mbeya

SERIKALI mkoani Mbeya imewataja viongozi wa Dini kuwa nyenzo muhimu inayopaswa kutumika katika kueneza elimu ya malezi sahihi kwa watoto kutokana na nafasi waliyonayo ndani ya jamii wanayoiongoza.

 

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,Dk Elizabeth Nyema alibainisha hayo alipomwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa huo kufungua  Kikao cha Tathimini ya Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM) ngazi ya Mkoa wa Mbeya kichohudhuriwa na wadau mbalimbali.

 

Nyema alisema kutokana na kuaminiwa kiroho mafundisho ya viongozi wa dini yamekuwa yakizingatiwa na waumini hivyo iwapo watashirikisha kikamilifua katika utekelezaji wa PJT-MMMAM ni wazi watoto watalelewa katika misingi ya ukuaji timilifu.

 

Alisema ni muhimu kwa viongoni wote wa dini wakawa na uelewa wa kutoka juu ya progarmu hiyo hususani kwenye maeneo yake makuu matano ambayo ni Afya bora,Malezi yenye muitikio,Fursa za ujifunzaji wa awali,Lishe bora na Ulinzi na Usalama.

 

Akizungumza mara baada ya kikao hicho,Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mbeya,Aika Temu alisema uanzishwaji wa vituo vya kijamii vya kulelea watoto mchana kwenye maeneo ya mikusanyiko katika kila halmashauri ni sehemu ya maadhimio yaliyofikiwa.

 

Alisema wajumbe waliiangalia kwa jicho la kipekee changamoto ya malezi wanayoyapata watoto wadogo wanaolazimika kwenda na wazazi weo kwenye maeneo ya biashara wanakojitafutia riziki ambako kuna mazingira yasiyo rafiki.

 

“Kupitia kikao cha leo tumeazimia kila halmashauri kuhakikisha inatenga maeneo kwaajili ya kuanzisha vituo vya kijamii vya kulelea watoto wadogo kwenye maeneo yenye mikusanyiko hususani sokoni.Tunaiona changamoto kubwa kwenye masoko unakuta mama yuko na mtoto toka asubuh mpaka jioni na hatujiu amekula lishe bora au toshelezi.” Alisema Temu

 

Afisa Ustawi huyo wa Mkoa alisema katika kikao kitakachofuata cha tathmini kila halmashauri italazimika kutoa taarifa ni kwa namna gani imetekeleza azimio hilo na kwa zitakazoonekana kusuasua hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa wahusika.


WAZEE MBARALI WATAKA USHIRIKI VYOMBO VYA MAAMUZI

 






Na Mwandishi Wetu,Mbarali 

HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya imeahidi kulifanyia kazi ombi la wazee wilayani huo waliotaka kundi hilo kushirikishwa kwa kuwa na wawakilishi kwenye vyombo vya maamuzi.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Raymond Mweli alitoa ahadi hiyo alipokuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani zilizofanyika kiwilaya katika Kata ya KongoloMswiswi.

 

Mweli alisema serikali inatambua na kuthamini mchango wa wazee katika jamii na itaendelea kutoa kipaumbele katika huduma mbalimbali za kijamii, ikiwemo huduma za afya na pia maombi na ushauri wanaoutoa.

 

Alisema ushirikishwaji wa wazee ni muhimu kutokana na uzoefu na busara walizonazo, ambao unaweza kusaidia katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo ya jamii.

 

Awali Katibu wa Baraza la Ushauri la Wazee la Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Michael Sanga akisoma risala ya wazee aliomba wazeekupewa nafasi ya kushirikishwa katika vikao vya maamuzi kuanzia katika ngazi za kata hadi halmashauri wakisema kundi hilo limesahaulika na halishiriki kama yalivyo makundi ya wanawake,vijana na walemavu.

 

“Tunaomba wazee washirikishwe katika vikao vya maamuzi, kuanzia Kamati za Maendeleo za Kata hadi vikao vya Halmashauri, ili tupate fursa ya kutoa mawazo na kushiriki katika kuleta maendeleo ya jamii.” Alisema Sanga.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza hilo wilayani humo, Hezron Kapwela, aliwataka vijana kutumia nguvu na uwezo walionao kujijengea maisha bora mapema, ikiwemo kujenga nyumba na kujiandaa kwa maisha ya uzeeni.

 

Kapwela alisema vijana wanapaswa kuanza maandalizi ya maisha ya baadaye wakiwa bado wana nguvu za kufanya kazi, ili kupunguza utegemezi kwa watoto wao wanapofikia uzee.

 

“Tunawaasa vijana jengeni nyumba mkiwa bado mna nguvu, msije mkawa kama wazee wanaolalamika sasa hivi kwamba watoto hawanijengei nyumba, wakati yeye alianza kuwa na nguvu na nguvu zimepotea sasa anaanza kutishia kutoa laana kwa watoto, hiyo laana hata Mungu haipokei,” amesema Kapwela.” Alisema Kapwela.