Na Mwandishi Wetu
BODI ya Chama cha Waigizaji(TDFAA) Mkoa wa Mbeya imemteua Ramadhan Shaban Ramadhan kuwa Katibu Mkuu mpya wa chama hicho baada ya nafasi hiyo kuwa wazi kwa zaidi ya miezi nane kufuatia aliyekuwa akiishikilia Florian Mwamboneke kuachia ngazi.
Mwenyekiti wa TDFAA Mkoa wa Mbeya,Andrew Mlelema(Chungwa) amesema Bodi ya chama hicho imempitisha Ramadhan kushika wadhifa huo baada ya kukaa na kujiridhisha juu ya sifa alizonazo ikiwemo ukongwe kwenye uongozi wa tasnia ya sanaa kwenye vikundi mbalimbali mkoani humo.
Mlelema amesema Bodi ilifikia hatua hiyo baada ya kuona nafasi hiyo inapwaya kwa kukosa mhusika hatua iliyokuwa ikisababisha utekelezaji wa majukumu mbalimbali ndani ya chama kuwa wa kusuasua.
“Kwa utaratibu mmoja wenu anapoondoka ni lazima mkaa chini kutafakari ili kumpata mtu sahihi wa kwenda kufanya nae kazi kwa pamoja.Tulikaa kama bodi ya TDFAA Mkoa wa Mbeya tukampendekeza Bwana Ramadhan Shaban Ramadhan tukaona anatufaa kuwa Katibu Mkuu wa chama chetu ngazi ya mkoa.” Amesema Mlelema
“Tumemuona ni mtu ana sifa nyingi za kipekee za kuitumikia nafasi hiyo kwakuwa kwanza ni muasisi wa tasnia katika makundi ya sanaa mkoani hapa hivyo anaujua mkoa vizuri.” Ameongeza zaidi
Mwenyekiti huyo amesema pengo lilikuwa kubwa kwakuwa katibu ndiye anayeratibu shughuli zote za chama na pia usimamizi wa kanuni za kikatiba,kuibua miradi sambamba na utunzaji wa kumbukumbu.
Amewataka wanachama na wadau wa sanaa ya uigizaji mkoani Mbeya kumpa ushirikiano katibu huyo mpya ili utendajikazi wake uwe na ufanisi kwa maslahi ya chama na sanaa ya uigizaji kwa ujumla.
Kwa upande wake Ramadhan Shaban Ramadhan amesema ushirikiano baina ya viongozi aliowakuta na wasanii wote utamwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufasaha zaidi na kuufanya mkoa kupaa katika tasnia ya uigizaji.
Kwa upande wake Shaida Mrabyo aliyeteuliwa kuziba nafasi ya mjumbe mmoja iliyokuwa wazi ameutaja mkoa wa Mbeya kuwa maeneo yaliyo na vipaji vingi vya sanaa ya uigizaji na kuahidi kuvivumbua na kuvikuza ili kuufanya mkoa uzidi kung’ara.
Nae Makamu Mwenyekiti wa chama hicho,Deborah Msungu(Shanifelix) amesema imani yao ni chama kufanya vizuri kwa sasa baada ya kumpata katibu aliye na uzoefu mkubwa kwenye sanaa pamoja na uongozi.

No comments:
Post a Comment