Na Mwandishi Wetu,Mbeya
VIJANA walio na umri wa
kati ya miaka 12 hadi 17 na wenye wazazi walio na uwezo wa kuwagharamia safari
ya kwenda Ulaya huenda wakanufaika na fursa ya kwenda kujinoa kisoka kufuatia
programu maalumu iliyoanzishwa kati ya Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini
na Taasisi ya Zodiac Eleven Football Club ya Uhispania.
Fursa hii inakuja baada
ya kufanyika kwa makubaliano kati ya Mbunge wa Mbeya Mjini,Patrick Mwalunenge
na uongozi wa Taasisi ya Zodiac Eleven
Football Club ya Bacelona nchini Uhispania ya kuendeleza na kukuza vipaji vya
vijana ambapo kwa kuanza vijana wa kiume wamepewa kipaumbele.
Kwa mujibu wa Afisa
mawasiliano Ofisi ya Mbunge Jimbo la
Mbeya Mjini,Antony Mswima programu ya kuwafanyia majaribio wachezaji kwaajili
ya kuwapima viwango vyao itafanyika Juni 15 na 16 kuanzia saa mbili hadi saa
tano asubuhi katika Uwanja wa Chuo cha Ufundi Ruanda Magereza jijini Mbeya
Katika kikao na waandishi
wa habari,Mswima amesema wachezaji watakaopatikana kupitia mchujo huo
watasafiri kwa gharama zao chini ya wakala wa Zodiac nchini mnamo Julai mwaka
huu hadi jijini Bacelona nchini Uhispani watakakokwenda kupikwa kupitia
programu mbalimbali za soka kabla ya kurejea nchini na kuendelea na maisha
mengine.
“Kupitia Zodiac Mh
Mwalunenge alifanya mazungumzo na
mtanzania ambaye ameishi Marekani na amefundisha soka la vijana kwa miaka
kadhaa na ameshiriki kupeleka wachezaji kadhaa nchini Uhispania,anaitwa kocha
Juma Maswanya.Mbunge ameamua kushirikiana naye na kuwaleta hapa Zodiac jijini
Mbeya kuja kutafuta vijana wenye vipaji vya kucheza mpira wa miguu.” Amesema
Mswima
“Wana Mbeya mjini
tutakuwa na upendeleo kwa sababu tuko nyumbani,inawezekana ikawa rahisi
kufika,lakini ikawa rahisi pia kusikia..vyovyote vile,lakini haitozuia mtu
kutoka Tanga..kutoka Dar es salaam…kutoka Kilimanjaro,na eneo lolote lile hapa
Tanzania.”
Kwa upande wake wakala
wa Zodiac nchini,Juma Maswanya amesema programu kama hizo ni muhimu kwakuwa
ndizo huwaibua vijana ambao baada ya kuendelezwa huwa na msaada kwenye timu
kubwa.
“Mazao ya wachezaji
wetu wakubwa Mbeya City bila huku chini hatuwezi kupata wachezaji bora,kwa hiyo
hilo ndilo dhumuni kubwa ambalo Zodiac itashirikiana na ofisi ya mbunge
kwaajili ya kusimamia mafunzo,kusimamia ubora wa mafunzo,na mpango wa hao
vijana utakaofanyika tarehe 15 na 16.Pia tunaangalia ushirikiano wa Zodiac na
vilabu vikubwa barani Ulaya na Amerika”
Naye Katibu wa Mbunge
wa Mbeya Mjini,Hakimu Edward alisema kuendeshwa kwa programu hiyo kunalenga
kuunga mkono juhudi za serikali za kukuza ajira kwa vijana kupitia sekta ya
michezo.
“Adhima ya serikali
yetu kupitia Wizara ya Habari,Utamaduni,sanaa na michezo chini ya Waziri Paul
Makonda wamewasilisha bajeti na kusisitiza umuhimu wa kuanzisha kliniki za
namna hii kwa lengo la kukuza na kuinua vipaji vya vijana wadogo.Kwa hivyo sisi
Mbeya mjini tukaona tusuport adhma hii ya serikali kwa kuwa watu wa mwanzoni
kabisa kuanzisha kliniki hii ya kusaka vipaji vya vijana wadogo.” Amesema
Maswali ya wadu wengi
juu ya fursa hii ni juu ya uwepo wa wazazi watakaomudu gharama za kuwasafirisha
watoto wao hadi ulaya hatua iliyozua gumzo ya kwanini waratibu wasianze na
kutafuta ufadhili ndipo kliniki iendeshwe kutokana na wazazi wengi kuwa na
kipato cha chini.












































