Na Mwandishi Wetu
Kamati ya Usalama barabarani Mkoa wa Mbeya imeitaka jamii kushirikiana katika utekelezaji wa mikakati ya kuzuia na kudhibiti ajali za barabarani kwa kufuata sheria za usalama barabarani.
Mulla ameahidi kufanya jitihada mbalimbali kama kamati kuhakikisha ajali za barabarani zinapungua lakini pia amewataka wana Mbeya kila mmoja kuwa balozi wa usalama barabarani na kuacha kuendesha vyombo vya moto bila kufuata sheria za usalama barabarani.
Naye, Mlezi wa kamati hiyo ambaye ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga amepongeza kazi na mikakati ya kamati hiyo katika kuzuia na kudhibiti ajali za barabarani.
Aidha, Kamanda kuzaga amesema kuwa miongoni mwa mikakati ni utoaji wa elimu ya usalama barabarani na matumizi sahihi ya barabara kwa makundi mbalimbali ya kijamii ili kuyajengea uelewa kuhusu sheria, alama na michoro ya usalama barabarani kwa lengo la kuzuia ajali zinazoweza kuepukika.
Kwa upande wake Katibu wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Mbeya, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Notker Kilewa ameeleza kuwa wameandaa kongamano la Wadau wa Usalama barabarani ili kutoa elimu ya usalama barabarani na kujadili masuala ya usalama barabarani.
Pia, SSP Kilewa ameeleza kuwa, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya litaendelea kuchukua hatua dhidi ya Madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani ikiwemo kuwafungia leseni na kuwafikisha Mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria lengo la kupunguza ajali.
No comments:
Post a Comment