Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Tuesday, June 2, 2026

MBARALI YATIKISA KWA USHINDI WA VIKOMBE 5 UMITASHUMTA MBEYA

 







Na Mwandishi Wetu,Mbarali

 

MSISIMKO wa Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) kwa ngazi ya Mkoa wa Mbeya yametamatika kwa wanafunzi takribani 120 kutoka Shule za Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali kuibuka kidedea kwa kuwa washindi wa kwanza mchezo wa mpira wa kikapu, washindi wa pili riadha na washindi nafasi ya tatu michezo ya mpira wa miguu, mpira wa wavu na mpira wa pete hatua iliyopelekea kuibuka na jumla ya vikombe vitano na vyeti vitatu

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Raymond Mweli amewapokea wanafunzi hao ofisini kwake leo Juni 02, 2026 na kuwapongeza kwa ushindi huo huku akiwaahidi kushirikiana na walimu, walezi na wazazi wao katika kuwaendeleza kitaaluma na michezo pia.

 

“Nilipokuwa nawaaga niliwasihi mkafanye vizuri na ninawapongeza hamjatuangusha, tutaendelea kulea vipaji vyenu kwa kushirikiana na walimu, walezi na wazazi wenu na tutatumia mashindano mbalimbali kuwaendelea kimichezo na kuitangaza Halmashauri yetu. Ni muhimu sana mkasome kwa bidii na muwe na maadili mema kwa ajili ya maisha yenu ya sasa na baadae na mtambue Taifa linawategemea”, amesema Mweli.

 

Aidha katika jumla  ya wanafunzi 120 waliowakilisha Wilaya ya Mbarali katika michezo hiyo, wanafunzi 15 wanaotokana na michezo mbalimbali wamebaki kwenye kambi ya Mkoa wa Mbeya kwa ajili ya maandalizi ya kuuwakilisha Mkoa katika ngazi ya michezo hiyo Kitaifa inayotarajiwa kuanza kufanyika Juni 06 mwaka huu Mkoani Iringa.

 

Kwa upande wake Kaimu Afisa Michezo wa Wilaya ya Mbarali, Bi. Mariam Mnozya ametoa shukrani kwa uongozi wa Halmashauri hiyo kwa kuwa nao bega kwa bega katika kila hatua kuanzia hatua za awali za maandalizi ya mashindano hayo ambapo amesema utayari wa uongozi huo imekuwa moja ya chachu ya mafanikio ya ushindi ambao umepatikana.

No comments:

Post a Comment