Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Saturday, June 13, 2026

WATAKAOMUDU GHARAMA KUNUFAIKA NA MPANGO WA KUPELEKA VIJANA BACELONA

 

Na Mwandishi Wetu,Mbeya

VIJANA walio na umri wa kati ya miaka 12 hadi 17 na wenye wazazi walio na uwezo wa kuwagharamia safari ya kwenda Ulaya huenda wakanufaika na fursa ya kwenda kujinoa kisoka kufuatia programu maalumu iliyoanzishwa kati ya Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini na Taasisi ya Zodiac Eleven Football Club ya Uhispania.

 

Fursa hii inakuja baada ya kufanyika kwa makubaliano kati ya Mbunge wa Mbeya Mjini,Patrick Mwalunenge na uongozi wa  Taasisi ya Zodiac Eleven Football Club ya Bacelona nchini Uhispania ya kuendeleza na kukuza vipaji vya vijana ambapo kwa kuanza vijana wa kiume wamepewa kipaumbele.

 

Kwa mujibu wa Afisa mawasiliano  Ofisi ya Mbunge Jimbo la Mbeya Mjini,Antony Mswima programu ya kuwafanyia majaribio wachezaji kwaajili ya kuwapima viwango vyao itafanyika Juni 15 na 16 kuanzia saa mbili hadi saa tano asubuhi katika Uwanja wa Chuo cha Ufundi Ruanda Magereza jijini Mbeya

 

Katika kikao na waandishi wa habari,Mswima amesema wachezaji watakaopatikana kupitia mchujo huo watasafiri kwa gharama zao chini ya wakala wa Zodiac nchini mnamo Julai mwaka huu hadi jijini Bacelona nchini Uhispani watakakokwenda kupikwa kupitia programu mbalimbali za soka kabla ya kurejea nchini na kuendelea na maisha mengine.

 

“Kupitia Zodiac Mh Mwalunenge  alifanya mazungumzo na mtanzania ambaye ameishi Marekani na amefundisha soka la vijana kwa miaka kadhaa na ameshiriki kupeleka wachezaji kadhaa nchini Uhispania,anaitwa kocha Juma Maswanya.Mbunge ameamua kushirikiana naye na kuwaleta hapa Zodiac jijini Mbeya kuja kutafuta vijana wenye vipaji vya kucheza mpira wa miguu.” Amesema Mswima

 

“Wana Mbeya mjini tutakuwa na upendeleo kwa sababu tuko nyumbani,inawezekana ikawa rahisi kufika,lakini ikawa rahisi pia kusikia..vyovyote vile,lakini haitozuia mtu kutoka Tanga..kutoka Dar es salaam…kutoka Kilimanjaro,na eneo lolote lile hapa Tanzania.”

 

Kwa upande wake wakala wa Zodiac nchini,Juma Maswanya amesema programu kama hizo ni muhimu kwakuwa ndizo huwaibua vijana ambao baada ya kuendelezwa huwa na msaada kwenye timu kubwa.

 

“Mazao ya wachezaji wetu wakubwa Mbeya City bila huku chini hatuwezi kupata wachezaji bora,kwa hiyo hilo ndilo dhumuni kubwa ambalo Zodiac itashirikiana na ofisi ya mbunge kwaajili ya kusimamia mafunzo,kusimamia ubora wa mafunzo,na mpango wa hao vijana utakaofanyika tarehe 15 na 16.Pia tunaangalia ushirikiano wa Zodiac na vilabu vikubwa barani Ulaya na Amerika”

 

Naye Katibu wa Mbunge wa Mbeya Mjini,Hakimu Edward alisema kuendeshwa kwa programu hiyo kunalenga kuunga mkono juhudi za serikali za kukuza ajira kwa vijana kupitia sekta ya michezo.

 

“Adhima ya serikali yetu kupitia Wizara ya Habari,Utamaduni,sanaa na michezo chini ya Waziri Paul Makonda wamewasilisha bajeti na kusisitiza umuhimu wa kuanzisha kliniki za namna hii kwa lengo la kukuza na kuinua vipaji vya vijana wadogo.Kwa hivyo sisi Mbeya mjini tukaona tusuport adhma hii ya serikali kwa kuwa watu wa mwanzoni kabisa kuanzisha kliniki hii ya kusaka vipaji vya vijana wadogo.” Amesema

 

Maswali ya wadu wengi juu ya fursa hii ni juu ya uwepo wa wazazi watakaomudu gharama za kuwasafirisha watoto wao hadi ulaya hatua iliyozua gumzo ya kwanini waratibu wasianze na kutafuta ufadhili ndipo kliniki iendeshwe kutokana na wazazi wengi kuwa na kipato cha chini.



No comments:

Post a Comment