Karibu katika blogu hii,kuwa mmoja wa wale wanaochangia na kujivunia mafanikio yake. Tunakualika kwa mikono miwili wasiliana nasi kwa simu 0756409597 au nyambojoachim@gmail.com

Saturday, June 13, 2026

WATAKAOMUDU GHARAMA KUNUFAIKA NA MPANGO WA KUPELEKA VIJANA BACELONA

 

Na Mwandishi Wetu,Mbeya

VIJANA walio na umri wa kati ya miaka 12 hadi 17 na wenye wazazi walio na uwezo wa kuwagharamia safari ya kwenda Ulaya huenda wakanufaika na fursa ya kwenda kujinoa kisoka kufuatia programu maalumu iliyoanzishwa kati ya Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini na Taasisi ya Zodiac Eleven Football Club ya Uhispania.

 

Fursa hii inakuja baada ya kufanyika kwa makubaliano kati ya Mbunge wa Mbeya Mjini,Patrick Mwalunenge na uongozi wa  Taasisi ya Zodiac Eleven Football Club ya Bacelona nchini Uhispania ya kuendeleza na kukuza vipaji vya vijana ambapo kwa kuanza vijana wa kiume wamepewa kipaumbele.

 

Kwa mujibu wa Afisa mawasiliano  Ofisi ya Mbunge Jimbo la Mbeya Mjini,Antony Mswima programu ya kuwafanyia majaribio wachezaji kwaajili ya kuwapima viwango vyao itafanyika Juni 15 na 16 kuanzia saa mbili hadi saa tano asubuhi katika Uwanja wa Chuo cha Ufundi Ruanda Magereza jijini Mbeya

 

Katika kikao na waandishi wa habari,Mswima amesema wachezaji watakaopatikana kupitia mchujo huo watasafiri kwa gharama zao chini ya wakala wa Zodiac nchini mnamo Julai mwaka huu hadi jijini Bacelona nchini Uhispani watakakokwenda kupikwa kupitia programu mbalimbali za soka kabla ya kurejea nchini na kuendelea na maisha mengine.

 

“Kupitia Zodiac Mh Mwalunenge  alifanya mazungumzo na mtanzania ambaye ameishi Marekani na amefundisha soka la vijana kwa miaka kadhaa na ameshiriki kupeleka wachezaji kadhaa nchini Uhispania,anaitwa kocha Juma Maswanya.Mbunge ameamua kushirikiana naye na kuwaleta hapa Zodiac jijini Mbeya kuja kutafuta vijana wenye vipaji vya kucheza mpira wa miguu.” Amesema Mswima

 

“Wana Mbeya mjini tutakuwa na upendeleo kwa sababu tuko nyumbani,inawezekana ikawa rahisi kufika,lakini ikawa rahisi pia kusikia..vyovyote vile,lakini haitozuia mtu kutoka Tanga..kutoka Dar es salaam…kutoka Kilimanjaro,na eneo lolote lile hapa Tanzania.”

 

Kwa upande wake wakala wa Zodiac nchini,Juma Maswanya amesema programu kama hizo ni muhimu kwakuwa ndizo huwaibua vijana ambao baada ya kuendelezwa huwa na msaada kwenye timu kubwa.

 

“Mazao ya wachezaji wetu wakubwa Mbeya City bila huku chini hatuwezi kupata wachezaji bora,kwa hiyo hilo ndilo dhumuni kubwa ambalo Zodiac itashirikiana na ofisi ya mbunge kwaajili ya kusimamia mafunzo,kusimamia ubora wa mafunzo,na mpango wa hao vijana utakaofanyika tarehe 15 na 16.Pia tunaangalia ushirikiano wa Zodiac na vilabu vikubwa barani Ulaya na Amerika”

 

Naye Katibu wa Mbunge wa Mbeya Mjini,Hakimu Edward alisema kuendeshwa kwa programu hiyo kunalenga kuunga mkono juhudi za serikali za kukuza ajira kwa vijana kupitia sekta ya michezo.

 

“Adhima ya serikali yetu kupitia Wizara ya Habari,Utamaduni,sanaa na michezo chini ya Waziri Paul Makonda wamewasilisha bajeti na kusisitiza umuhimu wa kuanzisha kliniki za namna hii kwa lengo la kukuza na kuinua vipaji vya vijana wadogo.Kwa hivyo sisi Mbeya mjini tukaona tusuport adhma hii ya serikali kwa kuwa watu wa mwanzoni kabisa kuanzisha kliniki hii ya kusaka vipaji vya vijana wadogo.” Amesema

 

Maswali ya wadu wengi juu ya fursa hii ni juu ya uwepo wa wazazi watakaomudu gharama za kuwasafirisha watoto wao hadi ulaya hatua iliyozua gumzo ya kwanini waratibu wasianze na kutafuta ufadhili ndipo kliniki iendeshwe kutokana na wazazi wengi kuwa na kipato cha chini.



ATUPWA JELA MIAKA 30 KWA KULAWITI

 


Na Mwandishi Wetu,Kyela

MAHAKAMA ya Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya imemuhukumu Agen Mwakyusa (34) Mkazi wa Kijiji cha Busoka Wilaya ya Kyela Mkoa wa Mbeya kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kulawiti alilolitenda kwa mama mwenye umri wa miaka 49 baada ya kumvamia akiwa amelala nyumbani kwake kisha kumwingilia kwa nguvu kinyume na maumbile.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu wa mahakama hiyo Paul Barnabas Juni 12, 2026 ambapo aAkisoma hukumu hiyo,Hakimu Barnabas alisema kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Januari 02, 2026 baada ya kufika nyumbani kwa mhanga ambaye anaishi peke yake majira ya usiku wa manane kisha kuvunja mlango na kuingia ndani na kutekeleza adhima yake ya kihalifu.

Mwendesha mashitaka wa serikali Wakili Sharon Sekemi akiwa mahakamani hapo alimuomba Hakimu kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa huyo ili liwe fundisho kwake na vijana wengine wa kiume wenye tabia kama ya mshitakiwa. 

Friday, June 12, 2026

Tanzania Yaeleza Mafanikio ya Ujumuishwaji wa Watu Wenye Ulemavu COSP19, Yaahidi Kuimarisha Upatikanaji wa Teknolojia Saidizi

 






Na Mwandishi Wetu

Serikali ya Tanzania imeeleza mafanikio makubwa iliyoyapata katika kuimarisha ustawi na ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu, huku ikisisitiza umuhimu wa kuongeza upatikanaji wa vifaa na teknolojia saidizi ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi.

Akihitimisha ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 19 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (COSP19-CRPD) uliofanyika New York, Marekani, Juni 11, 2026, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema teknolojia na vifaa saidizi vina mchango mkubwa katika kuwawezesha watu wenye ulemavu kuishi kwa kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.

“Ni muhimu kuendelea kuongeza upatikanaji na matumizi ya vifaa na teknolojia saidizi kwa watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi kwa usawa pia Serikali inaendelea kutekeleza kwa vitendo dhana ya ujumuishwaji kwa kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata fursa na haki kwa usawa katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi,” amesema Mhe. Mahundi.

Akizungumza kwa niaba ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Naibu Katibu Mkuu, Dkt. James Kilabuko, amesema ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo umeiwezesha nchi kujifunza uzoefu na mbinu mbalimbali za kukabiliana na changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu.

“Tanzania imepiga hatua kubwa katika uwezeshaji na ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu hivyo Kupitia mkutano huu, tumejifunza mbinu na uzoefu kutoka mataifa mbalimbali ambazo zitatusaidia kuimarisha zaidi juhudi zetu, lakini pia Serikali itaandaa mpango kazi mahususi kwa kushirikiana na wizara, taasisi na wadau mbalimbali ili kuendeleza utekelezaji wa masuala ya watu wenye ulemavu na kushughulikia changamoto zilizobainishwa wakati wa mkutano huu.,” amesema Dkt. Kilabuko.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Maghembe, amesema Tanzania imeendelea kuboresha huduma za afya za msingi kwa watu wenye ulemavu kwa kusogeza huduma karibu na wananchi kuanzia ngazi ya jamii, sambamba na kuboresha miundombinu ya afya na kuwajengea uwezo watumishi wa sekta hiyo katika utoaji wa huduma jumuishi.

Aidha, ameshauri Shirika la Afya Duniani (WHO) kuangalia uwezekano wa kutumia mifumo inayotumika katika upatikanaji wa chanjo na dawa muhimu duniani ili kuboresha upatikanaji wa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu, hususan katika nchi zinazoendelea.

Mkutano wa COSP19 umezikutanisha nchi wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu kujadili mafanikio, changamoto na mikakati ya kuimarisha haki, ushiriki na ustawi wa watu wenye ulemavu duniani

Barbara Hassan hapendi kusifia uwezo wake alipokuwa darasani

 

Aliyewahi kuwa mtangazaji wa Clouds FM,Couds TV na  Mjini FM,Barbara Hassan amewasihi wanafunzi kujenga tabia ya kusoma vitabu kwa lengo la kujijenga kujiamini huku wakiamini kuwa Ndani ya Ndoto Inawezekana.

 

Alitoa ujumbe huu wakati wa kufanyika kwa mdahalo Iduda High School iliyopo Kkata ya Iduda Jimbo la Uyole uliohudhuriwa na wadau mbalimbali wa elimu kutoka ndani ya mkoa wa Mbeya.

 

Mdahalo huo uliandaliwa na Taasisi ya Tulia Trust ulikiwa na mada isemayo “Maisha kabla ya umaarufu na safari ya mafanikio” huku kauli mbiu ikisema “Kutoka kuwa ndoto hadi uhalisia”* huku wanafunzi wakihimizwa Kujifunza, kujiamini na kujitegemea.


Thursday, June 11, 2026

TDFAA DAR ES SALAAM WAMLILIA MZEE ONYANGO

 


TANZANIA YAONGOZA MJADALA WA KIMATAIFA KUHUSU UIMARISHAJI WA HUDUMA NA UWEZESHWAJI KWA WATU WENYE ULEMAVU

 









Na Mwandishi Wetu

Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Balozi Togolani Mavura, ameongoza mjadala wa ngazi ya juu katika Mkutano wa 19 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (COSP19), uliojikita katika mada ndogo ya “Jamii Imara: Kuimarisha Mifumo ya Huduma na Msaada ili Kuhakikisha Uwezeshaji, Uhuru na Kujitegemea kwa Watu Wote Wenye Ulemavu.”

Akifungua mjadala huo, Mhe. Balozi Togolani amesema huduma na mifumo ya msaada ni msingi muhimu wa ustawi wa watu binafsi, jamii na uchumi kwa ujumla, huku akisisitiza kuwa utekelezaji wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu umeleta mafanikio makubwa duniani katika kipindi cha miaka 20 tangu kupitishwa kwake.

"licha ya hatua zilizofikiwa, bado watu wengi wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto za kupata huduma na msaada unaokidhi mahitaji yao, hali iliyodhihirika zaidi wakati wa janga la UVIKO-19 ambapo mifumo mingi ya huduma ilionekana kutokuwa imara na jumuishi vya kutosha hivyo ni muhimu kuimarisha huduma za usaidizi binafsi, huduma za urekebishaji na uendelezaji uwezo, vifaa saidizi, mifumo ya hifadhi ya jamii pamoja na huduma za kijamii zinazotolewa katika ngazi ya jamii katika kuwawezesha watu wenye ulemavu kufanya maamuzi yao wenyewe, kuishi kwa kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii, kiuchumi na kisiasa."Alisema Mhe. Balozi Togolani.

Aidha, amesema kuwa uwekezaji katika mifumo ya huduma na msaada si suala la maendeleo pekee bali ni wajibu wa kuheshimu haki za binadamu, huku akizitaka serikali, mashirika ya maendeleo, asasi za kiraia, mashirika ya watu wenye ulemavu na wadau wengine kushirikiana kwa karibu ili kuziba mapengo yaliyopo na kuharakisha utekelezaji wa sera na programu zinazolenga kujenga jamii jumuishi na himilivu.

Kwa upande wake Afisa Sheria kutoka kitengo cha Watu Wenye Ulemavu,Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Bw. Jacob C. Mwinula, akiwasilisha uzoefu wa Tanzania katika kuimarisha mifumo ya huduma na uwezeshwaji kwa watu wenye ulemavu wakati wa mjadala (Roundtable Discussion) ameeleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha ujumuishaji, kujitegemea na ushiriki wa watu wenye ulemavu kupitia sera, sheria, mifumo ya hifadhi ya jamii, huduma za afya, elimu jumuishi na uwezeshaji wa kiuchumi.


KAMATI YA USALAMA BARABARANI MKOA WA MBEYA YAWEKA MIKAKATI YA KUZUIA AJALI

 


Na Mwandishi Wetu

Kamati ya Usalama barabarani Mkoa wa Mbeya imeitaka jamii kushirikiana katika utekelezaji wa mikakati ya kuzuia na kudhibiti ajali za barabarani kwa kufuata sheria za usalama barabarani.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti Mpya wa kamati ya usalama barabarani Mkoani humo ndugu Pirmohamed Mulla katika kikao cha kwanza cha kamati hiyo tangu kuteuliwa na Naibu Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi mwezi Mei, 2026.

Mulla ameahidi kufanya jitihada mbalimbali kama kamati kuhakikisha ajali za barabarani zinapungua lakini pia amewataka wana Mbeya kila mmoja kuwa balozi wa usalama barabarani na kuacha kuendesha vyombo vya moto bila kufuata sheria za usalama barabarani.

Naye, Mlezi wa kamati hiyo ambaye ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga amepongeza kazi na mikakati ya kamati hiyo katika kuzuia na kudhibiti ajali za barabarani.

Aidha, Kamanda kuzaga amesema kuwa miongoni mwa mikakati ni utoaji wa elimu ya usalama barabarani na matumizi sahihi ya barabara kwa makundi mbalimbali ya kijamii ili kuyajengea uelewa kuhusu sheria, alama na michoro ya usalama barabarani kwa lengo la kuzuia ajali zinazoweza kuepukika.

Kwa upande wake Katibu wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Mbeya, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Notker Kilewa ameeleza kuwa wameandaa kongamano la Wadau wa Usalama barabarani ili kutoa elimu ya usalama barabarani na kujadili masuala ya usalama barabarani.

Pia, SSP Kilewa ameeleza kuwa, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya litaendelea kuchukua hatua dhidi ya Madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani ikiwemo kuwafungia leseni na kuwafikisha Mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria lengo la kupunguza ajali. 

TULIA TRUST UYOLE CUP 2026 KUENDELEA KUTIMUA VUMBI LEO

 


Tuesday, June 2, 2026

WASANII MBEYA KUCHANGIA DAMU JUNI 4

 


MBARALI YATIKISA KWA USHINDI WA VIKOMBE 5 UMITASHUMTA MBEYA

 







Na Mwandishi Wetu,Mbarali

 

MSISIMKO wa Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) kwa ngazi ya Mkoa wa Mbeya yametamatika kwa wanafunzi takribani 120 kutoka Shule za Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali kuibuka kidedea kwa kuwa washindi wa kwanza mchezo wa mpira wa kikapu, washindi wa pili riadha na washindi nafasi ya tatu michezo ya mpira wa miguu, mpira wa wavu na mpira wa pete hatua iliyopelekea kuibuka na jumla ya vikombe vitano na vyeti vitatu

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Raymond Mweli amewapokea wanafunzi hao ofisini kwake leo Juni 02, 2026 na kuwapongeza kwa ushindi huo huku akiwaahidi kushirikiana na walimu, walezi na wazazi wao katika kuwaendeleza kitaaluma na michezo pia.

 

“Nilipokuwa nawaaga niliwasihi mkafanye vizuri na ninawapongeza hamjatuangusha, tutaendelea kulea vipaji vyenu kwa kushirikiana na walimu, walezi na wazazi wenu na tutatumia mashindano mbalimbali kuwaendelea kimichezo na kuitangaza Halmashauri yetu. Ni muhimu sana mkasome kwa bidii na muwe na maadili mema kwa ajili ya maisha yenu ya sasa na baadae na mtambue Taifa linawategemea”, amesema Mweli.

 

Aidha katika jumla  ya wanafunzi 120 waliowakilisha Wilaya ya Mbarali katika michezo hiyo, wanafunzi 15 wanaotokana na michezo mbalimbali wamebaki kwenye kambi ya Mkoa wa Mbeya kwa ajili ya maandalizi ya kuuwakilisha Mkoa katika ngazi ya michezo hiyo Kitaifa inayotarajiwa kuanza kufanyika Juni 06 mwaka huu Mkoani Iringa.

 

Kwa upande wake Kaimu Afisa Michezo wa Wilaya ya Mbarali, Bi. Mariam Mnozya ametoa shukrani kwa uongozi wa Halmashauri hiyo kwa kuwa nao bega kwa bega katika kila hatua kuanzia hatua za awali za maandalizi ya mashindano hayo ambapo amesema utayari wa uongozi huo imekuwa moja ya chachu ya mafanikio ya ushindi ambao umepatikana.