
MTOTO Daudi Yisambi(9) mkazi wa kitongoji cha Sasyaka kijijini Masoko wilayani Mbeya hivi karibuni aliisherehekea siku ya Mtoto wa Afrika duniani kwa namna ya tofauti kwa yeye na familia yake kuwaomba wasamaria wema kumchangia fedha ili aweze kurejea hospitali kwaajili ya matibabu ya jeraha la moto lililomsababishia ulemavu.

Mtoto Daudi ambaye ni Yatima aliyefiwa na wazazi wote wawili alipatwa na jeraha la moto baada ya kulipukiwa na petroli alipokuwa akicheza na watoto wenzake Oktoba mwaka jana nyuma ya mguu wake wa kulia usawa wa goti.

Mtoto huyo ambaye hawezi kuzungumza kwa lugha ya Kiswahili bali Kimalila pekee alisema alilipukiwa na petroli walipokuwa wakicchezea mafuta hayo na wenzake wakijua ni mafuta ya taa lakini baadaye akajikuta anapata jeraha kubwa.
Alisema baada ya tukio hilo alipelekwa katika hospitali ya teule ya Ifisi iliyopo wilayani Mbeya ambako alitibiwa kwa takribani mwezi mmoja na kuruhusiwa kurudi nyumbani baada ya kupata nafuu na alipewa dawa ya kuendelea kupaka katika jeraha lake.

Alisema wakati akiendelea kuugua kidonda hicho akiwa anaishi nyumbani kwa bibi yake Mbushi Sendemle anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 75 na 80 ghafla mguu wake ulianza kujikunja kwa nyuma na hatimaye kidonda kikapona huku mguu ukishikamana kwa nyuma na sasa amepata ulemavu kwani hawezi tena kuunyoosha mguu huo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi,kaka wa Daudi aliyejitambulisha kwa jina la Shila Yisambi ambaye wanachangia baba lakini mama tofauti na ambaye pia ni mlemavu wa kutoona jicho moja alisema walishindwa kumrudisha mdogo wake hospitali kutokana na kukosa fedha.

“Ilikuwa vigumu kujua ni namna gani mdogo wangu aliungua na kupata jeraha kubwa katika mguu wake wa kulia kwani alikuwa akiishi na bibi yetu ambaye ni mzee sana.Baada ya matibabu ya awali pale Ifisi hatukuwa tena na fedha za kumrejesha hospitali.Pengine mdogo wangu asingepata ulemavu huu” alisema kaka wa Daudi.
Kaka huyo alisema kwa sasa wanaomba msaada kutoka kwa wasamaria wema ili waweze kumrejesha mdogo wake hospitali ili wataalamu waone uwezekano wa kumfanyia oparesheni mdogo wake ili ikiwezekana aepukane na ulemavu wa mguu huo kushikamana na aweze kutembea kama awali.
Mtoto Daudi kwa hivi sasa analazimika kutembelea mguu mmoja unaosaidiana na mti jambo linaloonyesha kuwa tarayi amepata ulemavu kutokana na kukosekana kwa fedha za kumrejesha hospitali anakoweza kufanyiwa upasuaji na akaweza kutembea.
Kutokana na ulemavu huo,hawezi kuvaa suruali hivyo hulazimika kushinda siku nzima akiwa amefunga kitenge kiunoni kwani ndilo vazi pekee linaloweza kuendana na umbile na ulemavu alionao kwa sasa.


Mwenyekiti wa kitongoji cha Sisyaka Iyela Sisala alisema baada ya kuguswa na tatizo la mtoto huyo ikilinganishwa na uwezo mdogo wa kiuchumi alionao bibi yake na ndugu zakre wa karibu,wakazi wa kitongoji hicho waliamua kuanza kuchanga na hadi wakati akizungumza na mwandishi wetu jumla sha shilingi 60,000 zilikuwa zimechangwa.
Lakini mwenyekiti huyo licha ya kusema michango ilikuwa ikiendelea kukusanywa,aliwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia kwa hali na mali kwa namna watakavyoguswa ili kuwezesha kumwokoa mtoto Daudi na ulemavu wa mguu.

Afisa mradi wa Kupinga ukatili wa Kijinsia(UWAKI) na dhidi ya watoto(VAC) kupitia kanisa la Anglikana Patrick Cossima aliyepo pichani na mtoto Daudi baada ya hoja ya mtoto huyo kuwasilishwa katika sherehe za maadhimisho ya mtoto wa afrika katika kata ya Masoko licha ya kuchangia kiasi chya shilingi 30,000 aliahidi kufuatilia kwa karibu akishirikiana na wadau wengine ili kumwezesha mtoto huyo kurejeshwa hospitali na kufanyiwa upasuaji.
No comments:
Post a Comment