Na Lyamba Lya Mfipa
SHILINGI milioni kumi zinatarajiwa kutumika kwaajili ya ukarabati wa Uwanja wa Kumbumbu ya Sokoine lengo likiwa ni kuuweka kweny hadhi stahiki ya kutumiwa kwa mashindano mbalimbali ikiwemo Ligi kuu ya Tanzania bara.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Mbeya, Langaeli Akyoo
alisema kuwa maboresho yanayofanyika ni pamoja na kupaka rangi kwenye
viti vya kukalia mashabiki, kufunga seng'enge mpya na kujenga vibanda vipya vya
benchi la ufundi.
Akyoo alisema ukarabati huo ni utekelezaji wa maelekezo ya barua waliyopokea kutoka Shirikisho la soka
Tanzania (TFF) ya kuwataka wamiliki hao kufanya maboresho kadhaa katika uwanja
huo ili kuendana na viwango vinavyohitajika.
"Tulipokea barua kutoka TFF ikitutaka, kufanya ukarabati na
maboresho kadhaa, ikiwemo kupaka rangi viti vinavyokaliwa na mashabiki, kufunga
seng'enge vizuri kuzunguka uwanja na kujenga upya vibanda vinavyokaliwa na
benchi la ufundi, na tayari zoezi hili tunaendelea nalo" alisema Akyoo
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mbeya, Patrick Mwalunenge, akiwa
ameongozana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (M-NEC), Ndele Jailos
Mwaselela na Katibu Mwenezi Christopher Uhagile jana walifika uwanjani hapo
kukagua maendeleo ya ukarabati huo unaoendelea.
Akiwa eneo la tukio Mwalunenge alisema kuwa wametenga zaidi ya
shilingi milioni 10 ambazo zitatumika kupaka rangi kuzunguka uwanja, na kudai
kuwa mpango uliopo ni kufanya ukarabati mkubwa ikiwa ni pamoja na kujenga
majukwaa ya mashabiki ili wasilowe na mvua pia kujenga vibanda vya kisasa vya
kufanyia biashara kuzunguka uwanja.
"Mpango wetu ni kuufanya uwanja wetu uvutie zaidi, kwahiyo
tunaendelea kutafuta wadau mbalimbali watakao tuunga mkono ili tufanye
maboresho makubwa sana kwenye uwanja wetu huu,
tutajenga majukwaa kuzunguka uwanja hata kama mvua inanyesha mashabiki
wasilowe, pia tuna mpango wa kufunga taa ili mpira uchezwe hata nyakati za usiku"
alisema Mwalunenge
Kwaupande wake Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (M-NEC),
Ndele Mwaselela alimpongeza Mwenyekiti Mwalunenge kwa jitihada hizo, kwa madai kuwa kazi hizi za kujitolea
zinahitaji zaidi moyo wa kujitoa.
Meneja wa uwanja Modestus Mwaluka alisema rangi inayopakwa
uwanjani hapo ni ya kijani na njano na kueleza kuwa mkandarasi aliyepewa kazi
hiyo anatarajia kukamilisha kazi hiyo ndani ya siku saba.



No comments:
Post a Comment